Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana leo Oktoba 14, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa maafisa wa kijeshi 32 kutoka Majeshi ya nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ambao wapo hapa nchini kuhudhuria mafunzo ya ukamanda na unadhimu kwenye chuo cha ukamanda na unadhimu cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kilichopo Duluti Mkoani Arusha.
Ujumbe huo uliojumuisha maafisa kutoka Majeshi ya Ulinzi ya nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania, ulitembelea Mkoa wa Dodoma Makao Makuu ya nchi kujionea na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu uchumi, Mazingira, Ulinzi, Usalama na maendeleo kwa ujumla.
Katika Mazungumzo yao, Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Rugimbana amewataka maafisa hao wa Majeshi kudumisha Umoja, Ushirikiano na Mshikamano baina ya nchi za Afrika, Tunu ambazo zililetwa na Waasisi wa Mataifa ya Afrika. Pia aliwataka Maafisa hao wa Majeshi kuendelea kuwa Wazalendo kwa kuzilinda nchi zao ili Afrika izidi kupiga hatua za maendeleo katika Nyanja mbalimbali.
Ujumbe huo ulipongeza uamuzi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kuihamishia Serikali Mkoani Dodoma na kusema kuwa kijiografia Dodoma kuwa katikati ya nchi kunaiwezesha Serikali kuwahudumia Watanzania kwa urahisi zaidi na hata kupelekea urahisi wa Watanzania kutoka Mikoa yote kufuata huduma mbalimbali za kiserikali Dodoma.
Luteni Kanali Katebe kutoka Zambia alimwelezea Mkuu wa Mkoa kuwa uamuzi wa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kuihamishia Serikali Mkoani Dodoma wao wanautazama kama moja ya mambo yatakayoongeza fursa kubwa za kiuchumi na kuchochea maendeleo kwenye ukanda mzima wa kati wa nchi ya Tanzania.
Jengo la Mkapa (Mkapa House) Barabara ya Hospitali ya Mkoa
Anuani ya Posta: 914 DODOMA
Simu: +255 26 232 4343/232
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@dodoma.go.tz
Hakimiliki©2016 GWF . Haki zote zimehifadhiwa.